Vyanzo 15-20 Vya Kupata Mtaji

Siku chache zilizopita tumejifunza Kuhusu Maana halisi ya Mtaji, Aina 15 za Mitaji Pamoja na Sababu kuu 4 za kwanini Mtaji ni Muhimu. Leo tunaenda kujifunza takribani vyanzo 15-20 Vya kupata mtaji. Enjoy!

Mtaji Pesa ni kitu cha muhimu katika biashara yeyote, Unahitaji Mtaji ili upige hatua moja kwenda nyingine. Kukosa ufahamu au maarifa ya jinsi ya kupata au kukuza mtaji unaweza kupelekea  Biashara yako kufa au kushindwa kufikia malengo.

Jifunze Hapa vyanzo ishirini vya kupata mtaji:

1. Kujiwekea Akiba (Personal savings)

    Moja ya kanuni ambayo imeelezwa na wataalamu wengi kama Robert Kiyosaki, George Clason kwenye kitabu chake cha THE RICHEST MAN IN BABYLON, Joel A. Nanauka kwenye kitabu chake cha TIMIZA MALENGO ni KUJILIPA WEWE KWANZA (PAY YOURSELF FIRST). Hakikisha kwenye kila pesa unayoipata unajilipa wewe kwanza kabla hujawaza kufanya mambo mengine. Kujilipa huku kunamanisha , ‘Kuweka akiba ya kiasi Fulani cha pesa unayoipata”. Hapa unaweza kuanza na asilimia yeyote kadri ya kipato au matumizi  yako . Mf; 10%, 20% n.k

    Jilipe wewe kwanza , Kuza Mtaji!

    2. Marafiki na ndugu

      Kabla hujatumia mbinu hii kama chanzo cha kupata mtaji ; kwanza  hakikisha umeweka mahusiano mazuri kwa rafiki au ndugu zako, pili hakikisha una chochote kitu cha kuanzia ambacho umekipata katika kujiwekea akiba ili waone uko serious kiasi gani na jambo lako. Tatu andika wazi ni kiasi gani unahitaji kama mtaji pamoja na matumizi yake kisha tafuta marafiki au ndugu ambao wanaweza kukuunga mkono .

      Kwa mfano; kama unahitaji million 10. Tafuta marafiki au ndugu 10 ambao wanaweza kukuchangia Million 1 @10.

      3. Uza Vitu ambavyo havikuingizii Pesa Moja kwa Moja

      Yawezekana unasema huna mtaji kumbe una vitu vya thamani ndani kwako ambavyo unaweza kuviuza ukavigeuza mtaji wa biashara yako. Kwa mf: TV, SIMU, RADIO N.K . kuuza vitu haimaanishi kwamba unafeli bali unajiandaa kuwekeza ili utengeneze PESA zaidi kupitia biashara yako.

      4. Ingia Ubia (Partnerships)

      Unaweza ukawa na wazo zuri  la biashara ila ukakosa mtaji pesa. Katika muktadha huu una chaguzi ya kuingia ubia na mtu mwenye pesa. Anaweza akawa rafiki yako au mwekezaji yeyote. Katika hali yeyote hakikisha unaweka makubaliano kisheria ili kuepusha migogoro ya badae pale mambo yanapoenda ndivyo sivyo!

      5. Uza Wazo ( Sell that idea)

      Pengine Huna Mtaji pesa kwa wakati huu lakini bado unaweza kuuza Mawazo ili ubadilishane na Pesa taslimu . Zipo njia nyingi za kuuza Mawazo!

      Kwa mfano: kama una kipaji cha utunzi unaweza kuuza nyimbo kwa wasanii, una kipaji cha kuandika Hadithi? Unaweza kuuza SCRIPTS Kwa wasanii wa Movies, una kipaji cha Ubunifu? Unaweza kutengeneza na kuuza designs mbalimbali, Una kipaji cha Mapishi? Unaweza kuandika kitabu chenye muongozo cha kupika chakula Fulani pendwa , unaweza kuuza Taarifa N.k

      Lazima Uwe tayari  kuanza na kidogo ulichonacho ili ukuze Mtaji wako!

      6. Anza na Wazo ( Start with the idea)

      Zipo Biashara zingine ambazo hazihitaji Mtaji Pesa moja kwa moja. Mara nyingi kinachotakiwa hapa ni Utayari wako, Nguvu zako, Kipaji Chako, Maarifa yako, Ujuzi wako, Muda wako pamoja na wazo lako tu.

      Siku Moja rafiki angu fulani  alinitafuta kuomba ushauri kuhusu , “Biashara gani afanye ambayo haina Mtaji Pesa kabisa”. Nilimueleza wazi kwamba hakuna biashara ambayo haitakuhitaji pesa lakini unapoanza na wazo ni rahisi kwako kupiga hatua moja kwenda nyingine. Kwa mfano; kama Wazo lako ni kuuza Nguo unachotakiwa kufanya ni kutafuta mfanyabiashara ambaye yupo kwenye biashara hiyo kwa muda mrefu na pengine anauza kwa Jumla, ongea naye akupe Bidhaa kisha kazi yako itakuwa kufanya udalali na mwisho wa siku unapata Cha juu (Faida baada ya mauzo). Kitu kizuri ni kwamba BIASHARA IMEHAMIA MTANDAONI, unachotakiwa kuwa nacho ni simu yako, bando lako na wafuasi (audience) ambao utawauzia bidhaa hizo. Na kitu cha Msingi ni kwamba lazima utengeneze jina  na nembo ya biashara ili watu wakuone upo serious na biashara yako!

      Baada ya siku chache, nilianza kuona rafiki angu anapost picha za nguo za kike STATUS! Hahaaaa.

      Anza na wazo lako, kuza Mtaji wako!

      7. Tangaza Huduma za wengine upate Gawio

      Mbinu hii ya kupata Mtaji kitaalamu/Kiingereza inaitwa MARKETING FOR COMMISSION au AFFILIATE MARKETING.

      Hapa unachofanya ni kuingia makubaliano na kampuni ndogo au kubwa kisha unatafuta masoko ya bidhaa zao, kwa kila mteja unayempata kuna gawio la asilimia Fulani unayopata.

      Hii ni njia nzuri sana ya kukuza mtaji kwasababu hauna stress ya wapi utapata bidhaa/Huduma. Bidhaa/Huduma zipo ila jukumu lako ni kuwa na ujuzi wa kutafuta masoko , kuuza pamoja na ujuzi wa networking.

      Kampuni kubwa kama AMAZON n.k  huwa zinatoa Link za Affiliate marketing, chukua Fursa hii kufuatlia mambo kwa kina!

      Kila la Kheri….

      8. Mtaji Kupitia Fedha ya Ubunifu:

        kabla haujakata tamaa kuwa wazo lako  haliwezi kufanikiwa kwa kukosa mtaji ni muhimu kufikiria nje ya Box.  Hakuna hasara unayopata katika kujaribu na kamwe huwezi kujua kama utafanikiwa mpaka UJARIBU!  Zaidi ya hayo, ni bora kushindwa kufanya kitu kuliko kufanikiwa bila kufanya kitu.

        Kutumia pesa za watu wengine ni fedha ya ubunifu, na inahitaji tu uwe mtu mwenye uadilifu na UAMINIFU. Watu wanaweza kukupa PESA ili utengeneze bidhaa au huduma na wewe unachotakiwa kuwapa ni  wanachohitaji tu. Unahitaji tu kuwa mbunifu na muaminifu.

        Mfano halisi ni biashara ya kuagiza mizigo nje ya nchi kama china , Dubai n.k : watu wanaweza kukuamini wakaweka oda za bidhaa wakalipa na pesa kisha wewe unaawagizia mizigo.  Vilevile kama ushafika hatua kubwa ya biashara , SUPPLIER anaweza kukupa bidhaa ukauza then ukamtumia PESA yake (Nimejifunza haya kwa Fred Vunjabei na wengine)

        Hata wewe unaweza kutumia Pesa ya wengine kama Mtaji.

        9. Tafuta Ajira.

          Pale ambapo mambo yanapokuwa magumu zaidi, kubali kutafuta kazi ya kuajiriwa ili uweze kutengeneza mtaji kupitia Ujira au posho unayopata. Hapa ni muhimu kuwa na malengo  makuu mawili muhimu; Kuajiriwa kupata Uzoefu wa kazi au kuajiriwa kupata Pesa au vyote kwa pamoja.

          10. Mikopo ya Asilimia 10 ya Halmashauri .

          Ipo sera serikalini ya kuwezesha vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia mikopo isiyo na riba. Hadi sasa sina taarifa zaidi kuhusu mikopo hii lakini  unaweza kufuatlia zaidi mwenyewe kwenye ofisi za halmashauri yako husika au kutembelea Tovuti ya ofisi ya Waziri mkuu kwa maelezo zaidi.

          11. Jiunge na VICOBA na SACCOS.

          Hii ni mifumo ya kifedha inayowawezesha wanachama kuchangia kiasi fulani cha pesa kila mwezi au kipindi fulani. Hii inaweza kufanyika kwa njia ya ushirika au shirika la akiba na mikopo. Hapa kuna ufafanuzi zaidi wa kila moja:

          VICOBA (Village Community Banks) ni mifumo ya akiba na mikopo ambapo wanachama wa jamii fulani, mara nyingi katika vijiji au maeneo ya mijini, hukutana kwa makubaliano ya kuchangia kiasi fulani cha pesa kila mwezi. Pesa zilizochangwa huchukuliwa na mwanachama mmoja kwa zamu kwa lengo la kutekeleza miradi au kusaidia mahitaji ya kifedha ya wanachama. Mfumo huu husaidia katika kuweka akiba na kutoa fursa za mikopo kwa wanachama.

          SACCOS (Savings and Credit Cooperative Organizations) ni taasisi za kifedha zinazomilikiwa na wanachama na kusimamiwa kwa pamoja. Wanachama wa SACCOS huchangia kifedha kwa kuchangia hisa na akiba ya kila mwezi,  kisha hutoa huduma za akiba na mikopo kwa wanachama wake. Kwa kawaida, SACCOS hufuata kanuni na miongozo ya usimamizi wa kifedha inayotolewa na mamlaka husika ya kifedha. Kwa ujumla, VICOBA na SACCOS zina lengo la kusaidia wanachama kufikia malengo yao ya kifedha kwa kutoa fursa za akiba na mikopo katika mfumo ulioboreshwa na kusimamiwa na wanachama wenyewe


          ITAENDELEA…